Thursday 10 July 2014

April fool na Uislam


Sitaki kuzungumzia asili ya April Fool day ili kufupisha mada yangu. Kila mmoja akae atafute asili ya April fool ni ipi basi muislamu wa kweli hakika hatokuwa pamoja na waongo na atajiepusha na kusema UONGO.

Ninachotaka kukizungumzia hapa ni hichi kitendo cha waislamu kusema Uongo kila ikifika tarehe mosi April. Uongo ni haramu haramu tena ni haramu. Na kuna makatazo makubwa ndani ya uislamu kuhusu Uongo. Leo muislamu anasema uongo kumwambia mwenzake je hakai akafikiria kuwa anaweza kumsababishia muislamu mwenzake kupata madhara? 

Leo unamwambia mtu aende sehemu kuna ajali au lolote je unajua mwenzako yuko katika hali gani wakati unampa habari hiyo? Halafu muislamu anacheka na kujidai kuwa amempata siku ya wajinga.

Mtume(swalla Allahu alayhi wasallam)anasema"Uongo ni haramu japokuwa ni maskhara"Katika jambo la kusema uongo waislamu tumekatazwa na tumetakiwa tuwe nalo mbali kabisa na kuna maonyo makali kutoka kwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam). Kutoka kwa Muaawiyah bin Haydah Amesema: " Nimemsikia Mtume Swalla Allaahu alayhi wasallam akisema:"Ole wake kwa anayehadithia jambo la uongo ili watu wacheke. Basi ole wake! Ole wake! (At-Tirmidhiy na amesema hii ni Hadiyth Hasan, na pia imepokelewa na Abu Daawuud)

JE VIPI MTUME (SWALLA ALLAHU ALAYHI WASALLAM) ALIKUWA AKIFANYA MZAHA

Kutoka kwa Ibn Umar (Radhiya Allaahu anhuma) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika mimi nafanya mzaha lakini sisemi ila tu yaliyo ya kweli" Attwabarany

Na tukumbuke kuwa miongoni mwa alama za mnafik moja wapo anapozungumza basi husema uongo. Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Alama za munaafiq ni tatu; akizungumza husema uongo, akitoa ahadi huivunja, akiaminishwa kwa kitu hufanya khiyana" Al-Bukhaariy na Muslim.

Ndugu zangu wa kiislamu tujiepusheni na jambo hili la kusema Uongo na tuwe wenye kuwakataza na wenzetu. Na mtu anaweza kusema nitatubia lakini mara hii lazima nimpate au hii mara ya mwisho. Basi wewe waza katika akili yako na je wakati unasema uongo malaika wa kutoa roho anakuja kuchukua roho yako na hujatubia. Nini utamjibu Allah wakati umerudi kwake unasema Uongo?

ALLAH ATUJAALIE WALE WENYE KUAMBIWA MAZURI NA KUYAFANYIA KAZI NA KUKATAZWA MABAYA NA KUYAWACHA"Aaamin.

“NA KUMBUSHA, KWANI UKUMBUSHO HUWAFAA WAUMINI”(51:55).

No comments:

Post a Comment