Wednesday 24 June 2015

Fadhila za kumsalia Mtume saw

Imeandikwa na alhidaaya.com

Allaah سبحانه وتعالى Anasema,

((إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا))

((Hakika Allaah Anamteremshia Rehma Mtume; na Malaika Wake (wanamuombea du'aa kwa vitendo vizuri alivyovifanya), Enyi mlioamini! Mswalieni (Mtume - muombeeni Rehma) na muombeeni amani)) [ Al-Ahzaab:56]

 

 

Hii ni amri kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى tumswalie Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na juu ya hivyo kuna fadhila kubwa kumswalia kwake kamailivyothibiti katika Hadiythi nyingi zifuatazo:

 عنْ عبد اللَّه بن عمرو بن العاص ، رضي اللَّه عنْهُمَا أنَّهُ سمِع رسُول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : ((من صلَّى عليَّ صلاَةً ، صلَّى اللَّه علَيّهِ بِهَا عشْراً))   رواهُ مسلم

Imetoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru bin Al'-Aasw رضي اللَّه عنْهُمَا kwamba kamsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anasema, ((Atakayeniswalia (atakayeniombea) mara moja Allaah Atamswalia (Atampa rahma) mara kumi)) [Muslim]

Subhaana Allaah! Hii ni fadhila tukufu kabisa kwamba Mola Aliyetuumba Atuswalie sisi waja wake mara kumi tutakapomswalia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم mara moja tu! Ukipima utaona fadhila hii haimkalifu mtu zaidi ya dakika moja!

 

Maana ya Swalah ya Allaah سبحانه وتعالى na Malaika Wake

Swalah ya Allaah سبحانه وتعالى  kwa waja Wake ni: Rahma na kuwasifu kwa Malaika.

Swalah ya Malaika kwa Waumini  ni: du'aa na kuwaombea Maghfirah.

عن ابن مسْعُودٍ رضي اللَّه عنْهُ أنَّ رسُول اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : (( أَوْلى النَّاسِ بي يوْمَ الْقِيامةِ أَكْثَرُهُم عَليَّ صلاةً)) رواه الترمذي وقال : حديثٌ حسنٌ

Imetoka kwa ibn Mas'uud رضي اللَّه عنْهُkwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلمamesema,

((Watu wa mwanzo kwangu (watakaokuwa karibu yangu) siku ya Qiyaamah ni wale wanaoniswaliasana))  [At-Tirmidhy na kasema ni Hadiythi Hasan]

 

Fadhila nyingine hii ya kuwa karibu kabisa na Mtume  wetu mpenzi  صلى الله عليه وآله وسلم. Nani asiyetaka kuwa na karibu naye siku ya Qiyaamah?

 عن أوس بن أوس ، رضي اللَّه عنْهُ قال : قالَ رسولُ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : (( إنَّ مِن أَفْضلِ أيَّامِكُمْ يَوْمَ الجُمُعةِ ، فَأَكْثِرُوا عليَّ مِنَ الصلاةِ فيه ، فإنَّ صَلاتَكُمْ معْرُوضَةٌ علَيَّ)) فقالوا : يا رسول اللَّه ، وكَيْفَ تُعرضُ صلاتُنَا عليْكَ وقدْ أرَمْتَ ؟ ، يقولُ : بَلِيتَ ، قالَ: (( إنَّ اللَّه حَرم على الأرْضِ أجْساد الأنْبِياءِ )) . رواهُ أبو داود بإسنادٍ صحيحِ

Imetoka kwa Aws ibn Aws   رضي اللَّه عنْهُ kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Siku iliyo bora kabisa kwenu ni siku ya Ijumaa, kwa hiyo zidisheni kuniswalia (siku hiyo) kwani Swalah zenu zinaonyeshwa kwangu)) Wakasema (Maswahaba) Ewe Mjume wa Allaah vipi Swalah zetu zinaonyeshwa kwako na hali utakuwa umeoza?  Akasema, ((Allaah Ameharamisha ardhi kuila miili ya Mitume)) [Abu Daawuud kwa isnaad ya Sahiyh]

 عنْ أبي هُريْرةَ رضي اللَّه عنهُ قال : قال رسُولُ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : (( رَغِم أنْفُ رجُلٍ ذُكِرْتُ عِنْدَهُ فَلَمْ يُصَلِّ علَيَّ))  رواهُ الترمذي وقالَ : حديثٌ حسنٌ .

 

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي اللَّهkwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلمamesema, ((Amepata khasara mtu ambaye nimetajwa kwake na hakuniswalia)) [At-Tirmidhiy na kasema Hadiyth Hasan]

 عنْ أبي هُريْرةَ رضي اللَّه عنهُ أنَّ رسُولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : (( ما مِنْ أحد يُسلِّمُ علَيَّ إلاَّ ردَّ اللَّه علَيَّ رُوحي حَتَّى أرُدَّ عَليهِ السَّلامَ )) . رواهُ أبو داود بإسناد صحيحٍ

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي اللَّهkwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلمamesema,

((Yeyote atakayeniswalia hurudishiwa roho yangu hadi nimrudishie salaam))[Abu Daawuud kwa isnaad ya Hasan]

 

Ni jambo la ajabu kwetu kuwa roho yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلمhurudishiwa kwa ajili ya kujibu salaam zetu tu.

 وعن علِيٍّ رضي اللَّه عنْهُ قال : قال رسُولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : (( الْبخِيلُ من ذُكِرْتُ عِنْدَهُ ، فَلَم يُصَلِّ علَيَّ )) رواهُ الترمذي وقالَ : حديثٌ حسنٌ صحيحٌ .

Imetoka kwa 'Aliy رضي اللَّه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلمamesema, ((Bakhili ni yule ambaye nimetajwa kwake na hakuniswalia))[At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

Bila shaka hakuna anayependa kuwa na sifa hiyo, na sio ubakhili wenye uhusiano na  fedha bali ni kwa kutokumswalia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم.

 

Vipi kumswalia Mtume?صلى الله عليه وآله وسلم

 عنْ أبي مسْعُود الْبدْريِّ ، رضي اللَّه عنْهُ ، قالَ : أَتاناَ رسُولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم ، وَنَحْنُ في مَجْلِس سعد بنِ عُبَادَةَ رضي اللَّه عنهُ ، فقالَ لهُ بَشِيرُ بْنُ سعدٍ : أمرَنَا اللَّه أنْ نُصلِّي علَيْكَ يا رسولَ اللَّهِ ، فَكَيْفَ نُصَّلي علَيْكَ ؟ فَسكَتَ رسولُ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم ، حتى تَمنَّيْنَا أنَّه لمْ يَسْأَلْهُ ، ثمَّ قال رسولُ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم  (( قولُوا : اللَّهمَّ صلِّ عَلى مُحَمَّدٍ ، وَعَلى آلِ مُحمَّدٍ ، كما صليْتَ على آل إبْراهِيم ، وَبارِكْ عَلى مُحَمَّد ، وعَلى آلِ مُحمَّد ، كما بَاركْتَ عَلى آل إبْراهِيم ، إنكَ حمِيدٌ مجِيدٌ ، والسلام كما قد عَلِمتم ))رواهُ مسلمٌ

Imetoka kwa Abu Mas'uud Al-Badriyرضي اللَّه عنْهُ ambaye amesema, alitujia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na sisi tulikuwa katika majlis (ukumbi) wa Sa'ad ibn 'Ubaadah رضي اللَّه عنْهُ Bashiyr ibn Sa'ad akamwambia, Allaah Ametuamrisha tukuswalie ewe Mjumbe wa Allaah, je, Vipi tukuswalie? Akanyamaza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم mpaka tukatamani kwamba asingelimuuliza. Kisha akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم((semeni: Allaahumma Swalli 'Alaa Muhammadin Wa 'alaa aali Muhammadin Kamaa Swallayta 'alaa aali Ibraahiym, Wa Baarik 'alaa Muhammadin Wa 'alaa aali Muhammadin Kama Baarakta 'alaa aali Ibraahiym Innaka Hamiydum-Majiyd. Na salaam kamamlivyofundishwa)) [Muslim]

 

Basi ndugu Waislamu tusiziache fadhila tukufu na nyingi kama hizo kwa kumswalia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kila mara, ndimi zetu ziwe daima zikimswalia na kufanya hivyo pia  inaingia katika fadhila za kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى. 

 

Allaahumma Turuzuku mapenzi Yako na mapenzi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Tujaaliye tuwe karibu yake katika Pepo ya Firdaws.  Allaahumma  Mpe Mtume Muhammad صلى الله عليه وسلم)  wasila, na fadhila, na Mfikishe daraja yenye kusifiwa, ambayo Umemuahidi.

 

Sunday 24 May 2015

MWEZI WA SHAABAN NA FADHILA ZAKE

Imeandaliwa na Raudhwah group

Mwezi wa Shaaban ni mwezi wa nane katika miezi ya kiislamu. Mwezi huu upo kati ya Rajab na Ramadhan. Rajab na Ramadhan ni katika miezi mitukufu. Ni mwezi ambao Muislamu anatakiwa ajihimu katika kufanya ibada. Pia ni mwezi ambao mja autumie katika kujiandaa zaidi na Ramadhan ili asiweze kupoteza fursa ya Ramadhan ikiwa Allah atamjaalia kufika. Pia husemwa kuwa umeitwa kwa jina la Shaaban kwa sababu ya waaarabu kutawanyika kwao katika kutafuta maji au katika mashambulizi baada ya kutoka mwezi wa Rajab. 

Miongoni mwa mambo ambayo yamependekezwa sana mja ayafanye ndani ya mwezi wa Shaaban ni kufunga. Kabla ya kuangalia ubora wa funga ndani ya Shaaban na vipi imethibiti, kwanza tuangalie umuhimu wa mja kufunga siku tu kwa ajili ya Allah. 

Imepokewa na Abi Said Al Khudri (Radhi za Allah ziwe ju yake) amesema: “Amesema Mtume wa Allah "Hakuna mtu yoyote anayefunga siku yeyote katika njia ya Allah Mtukufu isipokuwa Allah huuweka mbali uso wake na moto kwa siku hiyo aliyofunga miaka sabiini ". Imepokelewa na Bukhari na Muslim. Pia imepokewa na Amri Ibn Abass (Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Amesema Mjumbe wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) "Mwenye kufunga siku yeyote katika njia ya Allah moto huwa mbali naye kwa mwendo wa miaka mia moja”.Imepokelewa na Attbraniy

Hadithi tulizozitaja hapo juu zinaonesha wazi uzito wa mja kufunga siku moja tu kwa ajili ya Allah (subhanahu wata‘ala). Hivyo ndugu yangu Muislamu usiwe mzito kwa kusema hizi funga za sunna tu. Kimbilia funga za sunna ili uweze kupata kheri kama hizo. Na zifunge saumu zako kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (subhanahu wata‘ala).

KUPENDEKEZWA KUFUNGA KATIKA MWEZI WA SHAABAN NA FADHILA YA FUNGA HIYO

Kutoka kwa Bibi Aysha (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: “Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha kufunga hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) kufunga mwezi mzima kama alivyokuwa akifunga Ramadhaan, na sijamuona akifunga mara nyingi kama alivyofunga katika Shaabaan” Bukhaari na Muslim.

Kwa hakika Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akikithirisha zaidi kufunga ndani ya mwezi wa Shaaban kuliko miezi mengine yoyote ukitoa mwezi wa Ramadhan. Na katika hili Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) mwenyewe alieleza ni kwa nini hufunga zaidi ndani ya mwezi wa Shaaban. Imepokewa kutoka kwa Usama Ibn Zaid (Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Nilisema ewe Mjumbe wa Allah sikukuona ukifunga katika mwezi wowote katika miezi kama siku unazofunga katika mwezi wa Shaaban? Akasema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) Huo ni mwezi ambao watu wameghaflika nao baina ya Rajab na Ramadhan nao ni mwezi ambao (hurufaishwa) hupandishwa ndani yake amali za watu kwa Bwana wa Viumbe na napenda zipandishwe amali zangu na hali ni mwenye kufunga.” Imepokelewa na An-nasai.

Huyu ni kipenzi cha Allah ambae amesamehewa dhambi zake zilizopita na zinazokuja ila alikuwa akijihimu kwa kufunga ili a’amali zake zipelekwe kwa Allah hali ya kuwa amefunga. Je vipi mimi na wewe ambao daima ni wenye kumkosea Allah? Kwa nini na sisi tusijikurubishe kwa Allah kwa kufunga sana ndani ya mwezi wa Shaaban? Isitupite fursa hiyo na tujihimize katika suala zima la kufunga sisi wenyewe pamoja na watu wetu.

JE MTU AKITAKA KUFUNGA MWEZI MZIMA WA SHAABAN INASIHI?

Katika kauli yenye nguvu zaidi wanazuoni wanasema kuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) hakuwahi kufunga mwezi wowote kamili ambao ni sunna kufunga. Na hili linatokana na ushahidi kuwa imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas (radhi za Allah ziwe juu yake ) amesema "‘‘Mtume wa Allaah (swalla Allahu alayhi wasallam) hakuwahi kufunga mwezi wowote kikamilifu isipokuwa Ramadhan." (Bukhaari).

MLANGO WA KUKATAZWA KUFUNGA NUSU YA MWISHO YA SHAABAN

Imekatazwa kufunga katika mwisho wa Shaban kwa nia ya kutozikosa siku za mwanzo wa Ramadhani. Na hili linathbitishwa kuwa imeripotiwa katika Sahihi Bukhari kutoka kwa Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema: “Kufunga katika mwisho wa Shaaban kumekatazwa ili kuweka tofauti kati ya funga za Sunna na funga za faradhi.”

TANBIHI

Wale wenye tabia na mpangilio wa kufunga na ikawa siku za mwisho za Shaaban zimetokezea sambamba na siku ambazo mtu yule kawaida huwa anafunga, kama vile za Jumatatu na Alhamis, au funga ya Nabii Daud au imemkuta akiwa anaendelea kulipa saum ya deni basi hawa wao wanaruhusika kufunga.

MLANGO WA KUKATAZWA KUITANGULIA RAMADHANI KWA SAUMU YA SIKU MOJA AU MBILI

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhi za Allah ziwe juu yake) kutoka kwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema : “Asiitangulie mmoja wenu Ramadhani kwa saumu ya siku moja au mbili isipokuwa akiwa mtu alikuwa akifunga saumu yake basi na aifunge siku hiyo” Bukhari na Muslim.

Amesema Tirmidhi (3/69) na wanavyuoni wanaitumia hadithi hii, kwa kuchukia mtu kufanya haraka kufunga kabla kuingia mwezi wa Ramadhani. Ila mwenye kuzoea kufunga siku za jumatatu na alhamisi au siku tatu za kila mwezi au saumu ya Nabii Daud, ikawafiki saumu yake siku hiyo basi na afunge kama kawaida yake kwa sababu makatazo hayamuelekei yeye, kinyume cha mwenye kuanzia kufunga hali ya kuwa si wajibu kwake na wala hatakiwi kulipa wala si ada kwake, haitakiwi kwake kufunga.
Pia Yaumu Shakka kumekatazwa mtu kufunga. Yawmu Shakk (siku yenye shaka) ni ile siku ambayo watu hawana uhakika juu ya kuanza kwa Ramadhan, kwa sababu ya hali ya mawingu kufunga na mwezi kutoonekana au sababu nyinginezo.

Imepokewa kutoka kwa Swila Ibn Zufar “Tulikuwa kwa Ammar Ibn Yaser akaletewa mbuzi wa kuchoma akasema" Kuleni " akakaa mbali mmoja katika watu akasema “Hakika mimi ni mwenye kufunga” akasema Ammar “mwenye kufunga siku ambayo watu huitilia shaka basi amemuasi Abal Qassim (swalla Allahu alayhi wasallam). Bukhari.

Pia Muislamu anatakiwa ajihimu katika kufanya mambo mengine mbali mbali ya kheri kama kuswali swala za sunna, kuleta istighfaar na adhkaaar nyenginezo kwa wingi, kutoa sadaka kwa wingi na kheri nyengine. Haya yote mwenye kuyafanya yatamuandaa katika kuitumia Ramadhani yake vile ipasavyo.

UKUMBUSHO 

Wale wote wenye madeni ya swaumu, basi wasiwache kulipa madeni yao. Kwani hairuhusiwi mtu kuchelewesha kulipa deni la Ramadhani hadi ikaingia Ramadhani nyengine. Na mtu anaweza kuzilipa funga hizo ndani ya Shaaban kwa ushahidi kutoka kwa Mama wa Waumini Aysha (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema : “Ilikuwa ninazo siku za kulipa za Ramadhaan na sikuweza kuzilipa isipokuwa (katika mwezi wa) Shaaban.” Bukhaari.

Yeyote aliyekuwa na uwezo wa kulipa Swawm zilizompita kabla ya Ramadhaan (ya pili) kuingia na asifanye hivyo, basi atalazimika kuzilipa baada ya Ramadhaan (ya pili), pia analazimika kutubia na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku iliyompita. Huu ni msimamo wa Imam Maalik, Ash-Shafi’iy na Ahmad.

Na Allah ni mjuzi zaidi.

Tuesday 7 April 2015

Umoja wetu ni nguvu yetu


Kimsingi maana ya umoja na mshikamano kati ya Waislamu si kuwataka wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu kutupilia mbali itikadi zao, bali lengo kuu ni kujenga maelewano na mshikamano mbele ya adui wao wa pamoja. Naam, tofauti hizo za kimadhehebu zinaweza kujadiliwa kwa njia za kimantiki na busara katika vikao vya mijadala ya kielimu vya wanazuoni na maulamaa wa Kiislamu na kufikia nukta za wazi. Hapana shaka kuwa makelele na malumbano yasiyokuwa ya kielimu katika vikao vya umma kuhusu masuala ya kitaalamu hayawezi kuwa na matunda ya kuridhisha. Tunaweza kusema hapa kuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano katika umma ni kutolewa mijadala kama hiyo ya kielimu na kitaalamu kuhusu masuala ambao Waislamu wanatofautiana juu yake katika vikao vya umma na kwa njia ya kichochezi.
Dini tukufu ya Kiislamu inawalingania wafuasi wake wote kutumia akili na kutafakari na kuzidisha maarifa na elimu yao kadiri inavyowezekana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuwa na maarifa na elimu huzuia mifarakano na ukosefu wa maelewano. Inasikitisha kuona kwamba katika zama za sasa za mawqasiliano na utandawazi Waislamu wa madhehebu moja hawajui kabisa au wana maarifa finyu kuhusu itikadi za ndugu zao wa madhehebu nyingine ya Kiislamu. Upungufu huu wa maarifa kuhusu itikadi za madhehebu tofauti za Kiislamu umekuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano wa Kiislamu na umekuwa ukisababisha mambo mengi ya kusikitisha katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mwanafikra mmoja wa Kiislamu anasema: "Tishio linalowakabili Waislamu kutokana na hali ya kutofahamiana na kudhaniana vibaya ni kubwa zaidi kuliko lile linalotokana na tofauti zao za kimadhehebu."
Mwingine anasema kuhusu taathira mbaya za kutofahamiana kati ya Waislamu na mchango wake katika kukuza hitilafu kwamba: "Tofauti za kimadhehebu na kiitikadi ni jambo ambalo limekuwepo katika zama zote lakini jambo linalobadilika kila wakati na katika kila zama ni ukosefu wa maelewano na kutofahamiana kwa pande husika. Kwa sababu hiyo, moto wa ugomvi, malumbano na mifarakano huchochewa zaidi na zaidi."
Sheikh Muhammad Abu Zahra ambaye alikuwa miongoni mwa maulamaa wa chuo cha al Azhar cha Misri amesema:
"Tofauti na hitilafu zilizoko kati ya Waislamu zimepenya na kuingia zaidi katika fikra, hisia na nyoyo zao kutokana na taasubi na chuki za kikaumu na kimadhehebu kwa kadiri kwamba Muislamu mmoja humuangalia Muislamu mwenzake anayehitilafiana naye kifikra kama adui aliyeko mafichoni dhidi yake na si kama mtu mwenye mitazamo tofauti kama yeye anayefanya jitihada za kujua hakika ya sheria za Mwenyezi Mungu."

Amkeni wapendwa waislamu
umoja wetu ni nguvu yetu
Imeandikwa na Sheikh Rashid Ashukery.