Friday 24 October 2014

UKUMBUSHO KWA WENYE KUFANYA MIJADALA NDANI YA MITANDAO YA KIJAMII NA KUISHIA MATUSI AU KUZUA NDANI YA DINI

Makala Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wa ta‘ala) Muumba wa kila kilichomo katika ulimwengu huu. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Katika makala yangu ya leo nakusudia kupeleka nasaha zaidi kwangu binafsi pamoja na ndugu zangu wa kiislamu ambao hutumia mitandao ya kijamii kwa njia ya kujadiliana mambo mbali mbali ya kidini au ya kijamii.

Kumekuwa na maumivu makubwa ndani ya nafsi za waumini mbalimbali ambao huwa wanasoma maoni na mijadala ya dini ya waislamu ndani ya mitandao ya kijamii. Mijadala yenye hekima inafaa kwani inaleta funzo ndani ya jamii na kukosoana pale watu walipokosea. Ila mingi ya mijadala hiyo imekuwa haina heshima. Imekosa busara, na mwisho ni maneno machafu ambayo hata kuyaandika mfano wake siwezi. Leo nitajaribu kuyazungumza haya mambo kwa uchache ili tuweze kupeana tahadhari ili tusije kujuta siku ambayo mwanadamu hayatomfaa majuto yake. Miongoni mwa mambo yanayofanywa ni kama yafuatayo :

1-MATUSI YA NGUONI NA MANENO MACHAFU

Kwa hakika ukiwa unaangalia mijadala ndani ya facebook au whatsapp wengi wa watu huishia katika kutukanana na kutoleana maneno machafu. Ikiwa muislamu mwenzako hakubaliani na msimamo wako basi usimtukane wala usimwite majina mabaya au kumwambia maneno yasiyofaa. Tumia hekima katika kumfanya yule mtu aweze kukufahamu na aweze kukuelewa kile unachokikusudia. Lau angekuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam),masahaba zake na wema wengine waliopita kazi yao kutukanana tu katika kufikisha daawa kweli uislamu ungekuwa na hali gani?

Daawa yao na mijadala yao ilikuwa ni daawa iliyojengwa na misingi ya Allah (subhanahu wataala) iliyotajwa ndani ya Quraan “Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka”(16:125)

Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anaambiwa hata akijadiliana na wasiokuwa waislamu basi ajadiliane nao kwa namna iliyobora. Vipi baina ya muislamu kwa muislamu mwenzake? Vipi mazungumzo ya muislamu na muislamu mwenzake? Unadhani kuandika matusi na maneno yasiyofaa ndio utakuwa mtetezi wa uislamu? Hapana bali utakuwa ndio mpingaji wa aya za Quraan. Hebu tuangalie ndani ya Suratul Hujurati Allah ndani ya aya ya 11 Allah (subhanahu wataala) anasema “Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini.” Je haya yote waislamu tunayasahau?

Kumtukana muislamu mwenzako na asiyekuwa muislamu ni makosa ndani ya dini yetu. Tutumie lugha nzuri na laini baina yetu na baina ya wasiokuwa waislamu. Na yule ambae atakutukana basi wewe usirejeshe kwa tusi fahamu kuwa bado hajaijua haki siku akiiijua hatofanya hivyo.

Tuwe wapole na wenye kuheshimiana daima baina yetu.

2-KUZUSHWA KWA HADITHI ZA UONGO

Wakati watu wanapojadiliana wako watu huvuka mipaka na kuzusha yale yasiyokuwemo ndani ya dini. Wako wanaotunga hadithi na wako wengine wanaotoa fatwa kwa mambo wasiyokuwa na elimu nayo.

Ndugu zangu wa kiislamu tumuogopeni Allah (subhanahu wataala) tusitunge au tusiseme jambo ambalo halimo ndani ya Quraan wala sunna. Kama jambo hulijui ni bora kukaa kimya kuliko kuzua. Je unajua ni yapi yanayomsibu mwenye kuzua katika dini? Kutoka kwa Bibi Aisha(Radhiya Allahu anha) kuwa Mtume (Swalla Allahu alayhi wa aalihi wasallam) amesema : “Atakayezua akatia katika Dini yetu hii ambacho hakiko atarejeshewa mwenyewe.” (Al Bukhaariy na Muslim).

3-KUJITUKUZA KWA MTU KWA DHEHEBU LAKE AU ELIMU YAKE

Wako watu huwa wanajigamba na kujisifu kutokana na misimamo yake. Na huwa anaona ni rahisi sana kuwaambia waislamu wengine kuwa ni watu wa motoni na yeye na wenye kufuata madhehebu au misiamamo aliyokuwa nayo yeye ndio watu wa peponi na wako sahihi. Ni nani aliyekupa darja ya kuwaweka watu peponi na motoni? Ni nani aliyekwambia wengine uwadharau. Huo sio uislamu.

Tukhitalifiane lakini tusitoane kwenye uislamu wala tusiingizane motoni. Kwani hiyo ni kazi yake Allah (subhanahu wataala) peke yake. Bali sisi tukae kwa upendo nah uruma baina yetu. Allah (subhanahu wataala) anasema “Basi msijisifu usafi. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga na maovu.”(53:32).

Wako wengine wao hujiona ndio wenye elim una ndio wana haki ya kusema kila kit una wasemalo wao ndio sahihi ya wengine si sahihi. Huku ni kukosa kwa elim una adabu zake. Na inampasa muislamu ajiepushe na tabia hizo. Kwani kujionesha na kibri kuna makatazo makubwa ndani ya uislamu. Imepokelewa kutoka kwa Abdullah bin Masud (Radhi za Allah ziwe juu yake) kwamba Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema:"Hatoingia Peponi ambaye moyoni mwake mna chembe ya kiburi". Mtu mmoja akauliza: “Mtu hupenda nguo yake iwe nzuri na viatu vyake viwe vizuri (itakuwaje?)” Akasema: "Hakika Allaah ni Mzuri Anapenda Uzuri. Kiburi ni kukataa haki na kudharau watu)"Muslim

Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) :“Ninachokuogopeeni sana ni Shirki ndogo.)) Maswahaba wakauliza: "Ni nini hii Shirki ndogo, ewe Mtume wa Allah?" Mtume (Swalla Allahu alayhi waaalihi wasallam) akasema: Riya (kujionyesha).” [Imepokewa na Imaam Ahmad]

Nasaha zangu kwa waislamu tutumieni mitandao ya kijamii kwa uzuri. Daima tujue kuwa kila tunalolifanya linaandikwa na tutakuja kuyakuta katika kitabu chetu. Tuitumie mitandao hii kwa kujua kuwa Allah (subhanahu wataala) anatuona. Ikiwa binaadamu mwenzako unamuonea haya akuone ukiwa katika jambo ovu je huoni haya jicho la Allah likiwa linakuona unamuasi yeye na unafanya kinyume na alivyoamrisha?

Tutubieni kwa Allah (subhanahu wataala) toba ya kweli na tuache kabisa yale tuliyokuwa tunayafanya. Allah (subhanahu wataala) anasema “Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.”(50:19). Na anasema tena Allah (subhanahu wataala) “Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.”(36:65). Tukumbuke aya ya Allah (subhanahu wataala) isemayo ““Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.”(2:281).

Thursday 23 October 2014

JINSI YA KUITUNZA NDOA YAKO

Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

BISMILLAHI RRAHMANI RRAHIM

Namshukuru Allah kwa kunipa nafasi hii ya kuandika makala adhimu kama hii ambayo endapo itafanyiwa kazi na Allah سبحانه وتعالىakaitilia Tawfiq basi itakua ni sababu ya kuleta manufaa makubwa katika jamii. Kisha swala na salam zimuendee kipenzi chetu Mtume Muhammad (sawﷺ).

Ama baada ya utangulizi huo sasa nitaingia rasmi katika uwanja mpana wa ndoa. Na leo nimependa kuzielekeza nasaha zangu zaidi kwa upande wa kina dada Ni jinsi gani watazilinda ndoa zao.

Kama tunavyofahamu ya kuwa ndoa ni mafungamano ya hiari baina ya mke na mume kuishi kwa pamoja kwa mapenzi na huruma mpaka mwisho wa maisha yao. Hivyo kwa kutambua hili inabidi kila mmoja wao awe ni mwenye pupa katika kuyafanya mambo ambayo yatakayozidisha mapenzi ya mwenza wake ili lipate kupatikana lengo kuu la ndoa ambalo ni utulivu wa nafsi.

Leo nimependa kuwabainishia mambo ambayo endapo mke atamfanyia mumewe basi yatazidisha mapenzi makubwa kwa mumewe kwani wengi wetu tunashindwa kuyafahamu ima kwa ufinyu wa fikra zetu au kwa sababu ni wapya katika ndoa.
Yafuatayo ndio mambo yakumfurahisha mumeo ili kuiimarisha ndoa yako:

1-KUWA MTIIFU KWAKE KATIKA MEMA ANAYOKUAMRISHA.

Tukizungumzia suala la utiifu ninamaanisha kuyatekeleza yale anayoyataka uyafanye katika yale yanayoridhiwa na Allah (subhanahu wataala). Kila binaadamu huwa ana mambo anayoyapenda afanyiwe na anayoyachukia yani hapendi afanyiwe. Na hali hii inatofautiana kutokana na mtu mmoja na mwengine. Kwa kua kuna mambo ambayo wengine kwao ni kawaida lakini kwa wengine huwa ni kero..Mfano Kumwita mumeo majina mazuri ya mapenzi kama mpenzi, laazizi, honey wapo wanaume ambao wanapenda na wanajihisi fahari kwa kuitwa majina haya na wake zao ima wakiwa peke yao au mbele za watu. Lakini wengine huwa hawapendi au wanapenda waitwe majina mazuri wakiwa faragha na wake zao au hupendelea kuitwa majina yao halisi. Katika hali hii inabidi mke uende na namna mumeo anavyopenda na sio kumwita kwa namna upendavyo wewe. Nadhani nitakua nimefahamika katika hili.

Na Kumtii mume ni katika ibada takatifu sana ambazo humpeleka mwanamke peponi atakapoifanya na kumuingiza motoni atakapoenda kinyume nayo. Amesema Mtume(ﷺ) “Atakapo swali mwanamke swala zake tano(za faradhi), akafunga mwezi wake (wa ramadhani), akajihifadhi utupu wake (kwa stara inayotakikana na hakutoka nje ya ndoa yake), na akamtii mumewe ataambiwa siku ya kiama INGIA PEPONI KWA MLANGO UUPENDAO” Imepokelewa na Imam Ahmad.

Pia suala la kumtii mume ni katika ishara za imani. Kwani Allah Subhanahu wataala amesema katika Qur'an tukufu :((Enyi mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi...))(4:59) .Na katika wenye madaraka juu yetu sisi wanawake ni waume zetu ambao wamekubali kuchukua dhima kutoka kwa wazazi wetu. Hivyo ili kuipata imani ya kisawa sawa inabidi tuwe watiifu kwa Allah, Mtume na Waume zetu bila ya kuwasahau wazazi wetu kwani nao bado wanahaki na sisi. Allah atuwafikishe katika hili.

2-Ridhika na Alichonacho

Katika mambo ambayo huongeza mapenzi mno katika ndoa ni wanandoa kutosheka. Namaanisha kwamba kila mmoja awe ameridhika na hali yoyote atakayomkuta nayo mwenzake. Na hawi na sifa hii ila yule mwenye mapenzi ya dhati kwa mwenzake na pia mwenye imani katika kifua chake kwani hakika muumini siku zote hutosheka na alichonacho na kuridhia kwamba ni qadar ya Allah (subhanahu wataala) aliyomkadiria. Amesema Mtume (ﷺ) : (( Ridhia katika kile alichokugawia Allah utakua ni tajiri zaidi kuliko watu)) Attirmidhiy.

Na pia katika hadithi nyengine amesema Mtume (ﷺ) “Hakika amefaulu aliesilimu na akaruzukiwa kinachomtosheleza na akakinaishwa na Allah kwa kile alichomruzuku”. Muslim.
Hadithi hizi mbili zinatufundisha tuwe wenye kukinai na kile tulichoruzukiwa kwani ni sababu ya kufaulu hapa duniani mpaka kesho akhera.

3-MTUNZIE SIRI ZAKE

Hakika katika mambo yanayochukiza mbele ya Allah (subhanahu wataala) na yatakayomsababishia mtu kupata adhabu kali ni mke au mume kutoa siri za mwenzake kwa nia mbaya yaani kumfedhehesha. Kwani amesema Mtume (ﷺ) katika kuelezea hili: ((Hakika katika watu wenye nafasi mbaya siku ya Qiyaamah ni mwanaume anaemuendea mkewe au mke anaeendewa na mumewe (wakafanya tendo la ndoa) halafu akaeneza siri ile)). Muslim. Hadithi hii imemkemea kila mwanaume na mwanamke mwenye kueneza siri za mwenzake.

Hivyo ni wajibu wetu kuwa makini na hili kwani tutakapojiepusha nalo tutakuwa miongoni mwa wanawake wema.

4-MUAMINI MUMEO

Uaminifu baina ya wanandoa ni jambo muhimu sana linalopelekea ndoa kuwa madhubuti ama kinyume na hapo ndoa hulega lega na kupelekea kuvunjika. Katika suala la uaminifu kila mmoja anatakiwa kuwa ni muaminifu kwa mwenzake sawa sawa wapo karibu au mbali mbali.

Muamini mumeo na wala usimtilie mashaka kwani kumtilia mashaka kutakuondolea mapenzi katika moyo yako. Na pia usichukue hatua yoyote kwa jambo la kuambiwa haswa litakapotoka kwa mtu ambae anajulikana kwa tabia zake kuwa ni mfitinishaji na ni mchochezi baina ya ya watu. Kwani hata Allah Subhanahu Wataala ametuambia ndani ya Qur'an : ((Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda.)) 49: 6

Hivyo utakaposikia jambo lolote baya kuhusu mumeo ni bora kulihakikisha mwenyewe kwa macho au masikio yako ili usije ukaharibu ndoa yako kwa sababu zisizo na msingi.

5-JIPENDEZESHE KW AJILI YAKE

Tambua ewe dada wa kiislamu kwamba kujipamba kwa ajili ya mume wako ni ibada na utalipwa kupitia ibada hio. Utakapopenda kujipendezesha kwa ajili ya mumeo kwa namna mbali mbali zilizo za kheri (zinazoruhusiwa na sheria) basi mumeo hatakuchoka na kinyume chake atatamani kila anapopata fursa akimbilie ndani kwake kwani wewe mkewe ni sababu ya tulizo la macho yake na moyo wake.

Kinyume na hapo mke ukiwa hujipambi kwa ajili ya mumeo kwanza unapata madhambi kwa sababu wewe ndio unakua chanzo cha yeye kutafuta tulizo la jicho na moyo wake katika vilivyo vya haramu. Pili wewe kama utakua unajipamba nje ya nyumba yako basi nawe utakua unapata madhambi kwani Allah(subhanahu wataala) ametukataza kuyabainisha mapambo yetu ila kwa wale wasioruhusiwa kutuoa yani baba, kaka, mjomba, babu, baba mkubwa au mdogo na watu wanaokuhusu kwa damu au ulionyonya nao.

Allah(subhanahu wataala) anatuambia: ((Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.))24:31

Aya hii nadhani haihitaji ufafanuzi kwani yenyewe ilivyo imejitosheleza. Na ametukuka Allah kwani hatuamrishi ila lililo na kheri nasi na hatukatazi ila lililo na madhara nasi duniani mpaka kesho akhera.

Saturday 18 October 2014

SIMU ZA MIKONONI NA NDOA ZETU

Makala hii Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group.

Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wa ta‘ala) Muumba wa kila kilichomo katika ulimwengu huu. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Kwa hakika katika elimu aliyowajaalia Allah (subhanahu wataala) waja wake ni uvumbuzi wa mambo mbalimbali. Katika yaliyovumbuliwa mengine huwa na faida na mengine huwa na hasara. Simu ya mkononi ni miongoni mwa kifaa kilichovumbuliwa. Simu ina faida zake ikiwemo kurahisisha mawasiliwano baina ya mtu na mtu mwengine,kuweka ukaribu kwa familia au marafiki. Lakini kwa hakika kwa sasa simu ina madhara makubwa sana kwetu sisi. Na ni wachache sana ambao wamesalimika na fitna hizi au madhara yake.

Leo katika makala hii nakusuduia kuzungumzia jinsi simu za mikononi zinavyoharibu ndoa zetu na hata kupelekea kuvunjika kwa ndoa hizo. Ziko ndoa nyingi sana zimekwisha kwa wanawake kupewa talaka au kwa kuomba talaka na sababu kubwa simu za mikononi. Namuomba Allah ajaalie tawfiq iwe ni sababu kwa kila atakaesoma makala hii ya kujirekebisha pale alipokosea.

1-MAZUNGUMZO YA KIMAPENZI BAINA YA MWANANDOA NA MTU AMBAE SIO MWANANDOA MWENZAKE

Ni simu ngapi ndani yake zimekutwa na ujumbe wa kimapenzi. Ujumbe ambao mtu hajatumiwa na mke wake au mume wake. Tena huwa ni ujumbe wa mapenzi unaoshiria kuwa mke au mume ni mwenye kutoka nje ya ndoa yake. Linapotokea jambo hilo kwa wanandoa wako wengine hujifanya mafundi wa kusema uongo na wengine huishia kutoa maneno na kukosa jibu. Au mwanamme kujifanya yeye ndio bwana hatakiwi kuhojiwa. Na hata wengine huishia kupiga wake zao kwa sababu tu ya kushika simu yake.

Kwa nini mtu ukose uaminifu kwa mwanandoa mwenzako? Kwa nini utumiwe ujumbe wa kimapenzi na mtu asiyekuwa mume wako au mke wako? Hivi unadhani hesabu yako hutaikuta kwa Allah? Kwa nini simu imekuwa inawekwa password ambayo haambiwi mke ikiwa na mume au haambiwi mume ikiwa ni mke? Tunakwenda wapi enyi umma wa kiislamu? Kwa nini tunazifisidi ndoa zetu kwa kufuata matamanio ya nafsi zetu?

Napenda kutoa nasaha kwa wanandoa unapokuta ujumbe ambao unaashiria machafu kwa mume wako au mke wako basi usikimbilie kutoa maneno au kufanya yasiyostahiki. Kwanza uliza kwa hekima na uwe na subra yawezekana ni fitna tu imeundwa ili kukuharibieni ndoa zenu. Na haya yapo na tayari yameshavunja ndoa za watu kumbe ni jambo lililopangwa na kuzuliwa. Kwani Allah (subhanahu wataala) anasema “Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda.”(49:6). Ndio chunguza kwanza ili baadae usije kujuta kwa kumuingiza mwenzako kwenye makosa yasiyokuwa yake.

Na ewe uliyeoa au kuolewa acha tabia za kutoka nje ya ndoa yako. Umeaminiwa basi na wewe jiaminishe. Kwani hakika ni alama ya unafik yule anaeaminiwa akavunja uaminifu wake. Tambua kuwa Allah (subhanahu wataala) anakuona na tambua hakuna la siri kwake na ipo siku siri hiyo itatoka tena itakuwa ni siku ya majuto makubwa na fedheha. Na mwisho wake kuingia katika moto. Allah atuhifadhi. Allah (subhanahu wataala) anasema “Siku zitakapo dhihirishwa siri.”(86:9).

2-KUKUTWA NA PICHA ZISIZOKUWA NA HESHIMA NDANI YA SIMU

Siku hizi kuna whatsapp na facebook hizi nazo zina mchango mkubwa sana kuharibu ndoa zetu. Mwanamme anakuwa na picha za wanawake wakiwa hawana mavazi au mwanamke nae kukutwa na picha za wanaume. Je unadhani ni lipi ambalo mume wako au mke wako ataweza kulifahamu akikutana na hali hizo?

Picha kama hizi zinapatikana kwa aina mbili kuu kwanza ni picha zinazoezwa kwenye mitandao ya kijamii na watu ambao hawana khofu juu ya Allah na ni wenye kumuasi Allah (subhanahu wataala). Na pili huwa ni picha ambazo mwanamke au mwanamme ameziomba kwa watu wao ambao hufanya mambo ya haramu.

Umeoa au umeolewa kwa lengo upate utulivu wa nafsi. Na ukapewa uhuru uoe katika uwapendao na uolewe na yule umpendae. Sasa hili suala la kutafuta picha zisizokuwa na maana ten aza haramu zinatoka wapi?

Tena wanandoa wengine wanakutwa na picha hizo wakiwa na wanaume zao au wanawake zao ambao wanafanya nao maasi hali ya kuwa na wao wameolewa au wameoa? Ni wanawake wangapi au wanaume wangapi tayari wameshakutwa na kesi ya kukutwa na picha za wanaume au wanawake ambao sio jamaa zake ziwe za heshima au sio za heshima? Lazima mke au mume ataumia kwa sababu ya wivu. Haya yote yanasababishwa na simu zetu za mikononi. Tujiepusheni na tabia hii ili kuzilinda ndoa zetu.

3-KUJIFICHA NA SIMU WAKATI WA MAZUNGUMZO

Wengi wa wanandoa wenye kutoka nje ya ndoa zao huwa wanaogopa kuzungumza na simu mbele ya wake zao. Na ikiwa anazungumza huwa anajifanya huyo mtu hamjui kabisa au huwa anababika katika mazungumzo. Na wako wengine hasa wanaume wanapoingia kwenye nyumba zao huzima simu sababu kubwa husema hataki kukerwa ila ni wachache wenye ukweli. Wengi wao hukimbia kutumiwa ujumbe na wanawake au kupigiwa simu na wanawake wa haramu. Kwa nini simu ikiwa kwako tu ndio inazimwa? Basi itoe sauti iweke pembeni.

Itunze ndoa yako. Usiweke mazingira ya mwenzako kukutilia shaka na itakuja kupelekea kuondosha uaminifu kwenye ndoa yenu.

Kwa hakika mada hii ni refu na ina mifano mingi sana. Naomba niishie hapa na nitoe nasaha zifuatazo : Simu zetu zisituhadae hadi tukawa tayari kuvunja ndoa zetu na zikatupeleka pabaya siku ya Qiyama. Tumuogopeni Allah (subhanahu wataala). Hebu kaa na utafakari ni pesa ngapi umehonga kwa wanawake au umetumia kwa ajili ya wanawake wakati mke wako wa halali unae ndani nae ana shida zake nyingi sana? Tambua unatumia neema za Allah na utakuja kuulizwa juu ya neema hizo. Ewe mwanamke itunze ndoa yako na usikubali kuipoteza ndoa yako kwa kukosa uaminifu. Dunia ni hadaa na hesabu zetu zote tutazikuta kwa Allah. Tukumbuke aya ya Allah (subhanahu wataala) isemayo ““Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.”(2:281).