Tuesday 7 April 2015

Umoja wetu ni nguvu yetu


Kimsingi maana ya umoja na mshikamano kati ya Waislamu si kuwataka wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu kutupilia mbali itikadi zao, bali lengo kuu ni kujenga maelewano na mshikamano mbele ya adui wao wa pamoja. Naam, tofauti hizo za kimadhehebu zinaweza kujadiliwa kwa njia za kimantiki na busara katika vikao vya mijadala ya kielimu vya wanazuoni na maulamaa wa Kiislamu na kufikia nukta za wazi. Hapana shaka kuwa makelele na malumbano yasiyokuwa ya kielimu katika vikao vya umma kuhusu masuala ya kitaalamu hayawezi kuwa na matunda ya kuridhisha. Tunaweza kusema hapa kuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano katika umma ni kutolewa mijadala kama hiyo ya kielimu na kitaalamu kuhusu masuala ambao Waislamu wanatofautiana juu yake katika vikao vya umma na kwa njia ya kichochezi.
Dini tukufu ya Kiislamu inawalingania wafuasi wake wote kutumia akili na kutafakari na kuzidisha maarifa na elimu yao kadiri inavyowezekana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuwa na maarifa na elimu huzuia mifarakano na ukosefu wa maelewano. Inasikitisha kuona kwamba katika zama za sasa za mawqasiliano na utandawazi Waislamu wa madhehebu moja hawajui kabisa au wana maarifa finyu kuhusu itikadi za ndugu zao wa madhehebu nyingine ya Kiislamu. Upungufu huu wa maarifa kuhusu itikadi za madhehebu tofauti za Kiislamu umekuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano wa Kiislamu na umekuwa ukisababisha mambo mengi ya kusikitisha katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mwanafikra mmoja wa Kiislamu anasema: "Tishio linalowakabili Waislamu kutokana na hali ya kutofahamiana na kudhaniana vibaya ni kubwa zaidi kuliko lile linalotokana na tofauti zao za kimadhehebu."
Mwingine anasema kuhusu taathira mbaya za kutofahamiana kati ya Waislamu na mchango wake katika kukuza hitilafu kwamba: "Tofauti za kimadhehebu na kiitikadi ni jambo ambalo limekuwepo katika zama zote lakini jambo linalobadilika kila wakati na katika kila zama ni ukosefu wa maelewano na kutofahamiana kwa pande husika. Kwa sababu hiyo, moto wa ugomvi, malumbano na mifarakano huchochewa zaidi na zaidi."
Sheikh Muhammad Abu Zahra ambaye alikuwa miongoni mwa maulamaa wa chuo cha al Azhar cha Misri amesema:
"Tofauti na hitilafu zilizoko kati ya Waislamu zimepenya na kuingia zaidi katika fikra, hisia na nyoyo zao kutokana na taasubi na chuki za kikaumu na kimadhehebu kwa kadiri kwamba Muislamu mmoja humuangalia Muislamu mwenzake anayehitilafiana naye kifikra kama adui aliyeko mafichoni dhidi yake na si kama mtu mwenye mitazamo tofauti kama yeye anayefanya jitihada za kujua hakika ya sheria za Mwenyezi Mungu."

Amkeni wapendwa waislamu
umoja wetu ni nguvu yetu
Imeandikwa na Sheikh Rashid Ashukery.