Thursday 18 December 2014

NASAHA MUHIMU SANA KWA WATUMIAJI WA SIMU ZA MIKONONI,FACEBOOK,WHATSAPP NA MITANDAO MENGINE YA KIJAMII


Anasema Allah (subhanahu wataala) “Na tukambainishia zote njia mbili“(Suratul Balad :10). na akasema tena “Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.”(Suratul Insaan :3).

Aya mbili za juu zinaonesha ni vipi ambavyo Allah (subhanahu wataala) amempa uhuru wake mwanadamu. Allah (subhanahu wataala) amembainishia mwanadamu njia mbili. Na akamwambia njia hii ukiifuata basi utapata radhi zangu na ukiikataa njia hii ukafuata njia nyengine basi huko utapata ghadhabu zangu. Allah (subhanahu wataala) akamuacha mwanadamu achague mwenyewe ni wapi pakufuata. Na kumuacha huku si kwa lengo jengine ila ni kumpa mtihani. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi.” (Suratul Mulk :2).

Wengi wa wanaadamu wameghafilika na uhuru walopewa. Na hakuna kinachowaghafilisha ila ni pumzi za dunia na starehe zake. Badala ya kufuata njia ya kheri amekuwa akiifuata njia ya shari na akafanya matamanio yake ndio mola wake. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake”(Suratul Jaathiyah : 23).

Na mwanadamu huwa anajua kama amepewa uhuru huo. Kwani hata anapokumbushwa neno la Allah au kukatazwa usifanye hiki kibaya hujibu kaburi lako au langu? Pesa ninayoitoa yangu ya yako? Wewe inakuhusu nini? Yote hayo ni miongoni mwa majibu yake. Lakini kwa uwezo wa Allah tusichoke katika kuwakumbusha na kujikumbusha.

Sasa tuangalie uhuru wake mwanadamu na kipi ataenda kumjibu Allah (subhanahu wataala)?

1-Muislamu amepata simu kutoka njia yoyote ile iwe ya halali au ya haramu. Lengo la simu hiyo ni kwa ajili ya mawasiliano. Anajua mwenyewe yawe ya kheri au ya shari. Lakini hebu ajiulize yafuatayo : Mauti yakimfika na simu yake iko mkononi mwake au mfukoni mwake, Je Allah (subhanahu wataala) atakuwa radhi na yeye?

Ili Allah (subhanahu wataala) awe radhi nae maana yake kusikuwemo na lolote lile la haramu la kumkera Allah (subhanahu wataala).

Au Allah (subhanahu wataala) hatokuwa radhi nae kwa sababu ndani ya simu yake imejaa message za matusi,mapenzi na mazungumzo ya haramu? Au ndani ya simu yake imejaa namba za wanaume au wanawake ambao husema ni wapenzi wake wa haramu? Au ndani ya simu yake kuna video za ngono na nyimbo? Au yeye ameoa au ameolewa lakini hutumia simu yake kutoka nje ya ndoa? Au hutumia simu yake kuwadhulumu watu na kufanya mambo ya riba au kuiba?

Nini atamjibu mwanadamu huyu Allah (subhanahu wataala)? Je anajitengenezea njia gani kwa Allah? Hebu jiulize masuala haya sasa hivi ikiwa mtu atafikwa na mauti. Je simu yake inamridhisha Allah?

2-Muislamu anatumia facebook.Ikiwa facebook hiyo inatumika katika kheri na kwa ajili ya Allah pongezi kwako ewe ndugu yangu wa kiislamu. Je ikiwa facebook hiyo muislamu unaitumia katika dhambi nini utamjibu Allah (subhanahu wataala) baada ya kufikwa na mauti?

Malaika wa roho akija kukutoa roho huwa hakupi fursa ukafute picha za wanawake au wanaume ulizotumiana na wenzako. Hakupi fursa ukafute picha za uchi ulizopiga na kumtumia mwanamme au mwanamke. Hakupi fursa ukafute mazungumzo yako ya kimapenzi katika njia ya haramu. Hakupi fursa ukafute comment zako za matusi kwa watu. Hakupi fursa ukafute message zako za matusi ulizowatumia watu. Hakupi fursa ukafute yale uliyoyaweka katika kurasa yako na watu wanaona?

Je umeona uzito wake? Je kweli unalo jibu la kumjibu Allah (subhanahu wataala) ikiwa hali yako ni hiyo sasa? Malaika wa roho anarejesha roho kwa Allah inbox yako facebook imejaa picha na mazungumzo ya haramu. Facebook yako umeweka nyimbo na mambo mengine ya kuwafurahisha wanaadamu na kumkera mola wa walimwengu na ulimwengu. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.” (Suratu Nnuur:19).

3- Muislamu anatumia whatsapp. Ikiwa ni katika njia ya kheri basi Allah akuridhie. Je ikiwa ni kwa shari?
Muislamu husambaza nyimbo ndani ya whatsapp. Husambaza video za ngono na picha za ngono  iwe video hiyo kajirikodi yeye au picha hiyo kajipiga yeye au mwengine. Tena wengine husema wanaficha sura. Je unamficha mpaka Allah (subhanahu wataala) anaejua mpaka yaliyojificha ndani ya kifua chako?

Muislamu husambaza haramu yoyote ile na huku anacheka akiona anawafurahisha wenzake. Tena wako wanaosifiwa fulani kila siku hakosi jipya. Naam sifa za kidunia zimemlevya ila je anajua kuwa kila atakaengalia yale aliyotuma anapata dhambi? Je hajiulizi akifa leo watu wataangalia video zile au picha ile kwa miaka mingapi na ni wa ngapi wataangalia? Je anajua na yeye anapata dhambi kwani alichangia kusambaza uchafu? Allah (subhanhu wataala) anasema "Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua."(Suratul Ankabut:13).

  Wengine husambaza aibu za watu kwenye whatsapp,matusi na habari za uongo. Je malaika wa kutoa roho anakuja kuchukua amana ya roho. Nini atamjibu mola wa viumbe vyote?

Isituhadae dunia na vilivyomo ndani yake. Zisituhadae pumzi na kusahau akhera zetu. Tusifuate matamanio ya nafsi zetu. Tusije kujuta wakati huo wakati ambao majuto hayana tena faida. “Na watasema: Lau kuwa tungelisikia, au tungelikuwa na akili, tusingelikuwa katika watu wa Motoni!." Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni!.” Suratul Mulk : 10-11)

Turudini kwa Allah (subhanahu wataala) na tukae katika njia yake. Hata yule ambae kishayafanya basi akitubia kwa Allah tawba ya kweli basi Allah atamsamehe. Allah (subhanahu wataala) anasema “Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu”.(Suratu Zumar : 53).
ALLAH TUJAALIE WALE WENYE KUAMBIWA MAZURI NA KUYAFANYIA KAZI NA KUKATAZWA MABAYA NA KUYAWACHA"Aaamin.

“Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.”(Suratul Baqara:281).

Makala Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group.

No comments:

Post a Comment