Friday 26 December 2014

SHEMEJI NA MIPAKA YAKE YA KISHERIA NDANI YA UISLAMU


Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wa ta‘ala) Muumba wa kila kilichomo katika ulimwengu huu. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Shemeji huwa ni ndugu wa kiume wa mume kwa mke au ni ndugu wa mke kwa mume. Watu hutumia neno shemeji katika kuonesha uhusiano uliokuwepo baina yao. Lakini leo hebu tuangalie ni yapi yanayofanywa ndani ya jamii za kiislamu baina watu na shemeji zao na uharamu wake ndani ya uislamu.

Kwanza tambua ewe ndugu yangu mpenzi kuwa shemeji yako si mahaarim yako(anaweza kukuoa au unaweza kumuoa). Wako watu hudhani kuwa shemeji yake hana neno. Hayo ni makosa lazima sheria za kiislamu zichungwe wakati wa kukaa nae.

Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)“Tahadharini na kuingia kwa wanawake(kuingia majumbani mwao)”. Akaulizwa: “Je, ndugu wa mume [shemeji])”. Akasema (Swalla Allahu alayhi wasallam): “Huyo (shemeji) ni mauti” (Bukhari na Muslim).

Miongoni mwa mambo yasiyofaa kufanywa mbele ya shemeji na jamii zetu wanajisahau nayo:

1-Kutovaa hijabu ya kisheria. Wako baadhi ya waislamu wanadhani kuwa mbele ya shemeji yake anaweza kuvaa vyovyote. Kwa mfano mwanamme unamkuta amevaa bukta haisitiri magoti au amekaa tumbo wazi mbele ya mke wa kaka yake. Au mwanamke kuvaa nguo za kubana au kutembea bila ya stara kichwani au vazi lolote lile analovaa ndani. Hayo yote ni makosa na hayafai ndani ya uislamu.

Tena la kusikitisha waume au wake wamekaa kimya wakidhani na wao ni sahihi au wanajua ovu bali wananyamaza. Na hili ni miongoni mwa sababu zinazopeleka kusikia kesi amemchukua mke wa kaka yake au mume wa dada yake. Ndio inachangia mume au mke anaona umbo la shemeji yake. Unadhani nini kitatokea?

Anasema Allah (subhanahu wataala) “Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.”(Suratu Nnur : 31).

Aya iko wazi hapo kuwa shemeji hajatajwa. Kwa nini waislamu tuige mila za mayahudi na manasara?
Pia imekatazwa kujipamba mbele ya shemeji. Kama tulivyosema yeye si maharimu yako hivyo hatakiwi akuone unapojipamba au ulivyojipamba. Ila hili ni msiba kwa wanawake wa sasa maana wanajipamba na wanaranda majiani waonekane na kila mwanamme.

2- Kukaa faragha au kutoka pamoja faragha. Shemeji si maharim yako. Hivyo haipaswi mukae faragha baina yenu. Ila jamii ilivyojisahau unamkuta mtu anarudi harusini usiku anaenda kuchukuliwa na shemeji yake. Wako peke yao wanarudi. Mtu na shemeji yake wanatoka peke yao bila ya maharim baina yao wanakwenda safari zao na kurudi. Haya nayo ni makosa. Na mume au mke ndio wa kwanza kusema mpeleke shemeji yako safari zake.

Kwa nini makosa? Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anasema: “Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi asikae peke yake na mwanamke asiyekuwa maharimu yake pamoja naye, kwani watatu wao ni shetani” (Ahmad).

Mtume (Swalla Allahu alayhi wasallam) amesema: "Hawi faraagha mmoja wenu pamoja na mwanamke ila awepo Mahram wake" (Bukhari Na Muslim)

Hadithi zinaonesha moja kwa moja kuwa haya yenye kufanywa hayafai. Shemeji si maharim yako. Bora jamii ikuone tofauti kwa kufuata sheria za Allah (subhanahu wataala) kuliko kuwaridhisha wao na unamkera Allah (subhanahu wataala).

3-Miongoni mwa makosa mengine yanayofanywa ni kwa kupeana mikono wakati wa kusalimiana au waki zungumza, Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allahu ‘alayhi wasallam): “Mmoja wenu kuchomwa [kudungwa] katika kichwa chake (na katika Riwaya: (cha mwanamme) kwa msumari au sindano ya chuma ni bora kwake kuliko kumgusa mwanamke asiyekuwa halali kwake.” Imepokelewa na Atw-Twabaraaniy.

Mtu na shemeji yake wanapiga picha huku wameshikana mikono au kamkumbatia shemeji yake. Au mwanamke anapiga picha na shemeji yake wakati mwanamke amevaa vazi lisilo la kisheria. Wenyewe wanasema wanaishi kizungu. Ila tambua hayo yote ni makosa. Na haitakikani waislamu tuchukue mila za mayahudi na manaswara tujipambe nazo. Ni lazima tujiepushe nazo.Maana mambo haya yanafanywa na wasiokuwa waislamu na muislamu anafanya ili na yeye aonekane anaenda na wakati. Ila atambue yamekatazwa katika uislamu.

Na wala hatusemi mtu asizungumze na shemeji yake. Wazungumze wakae vizuri ila iwe chini ya muongozo uliowekwa na dini yetu. Na kufuata sheria za kiislamu ni kujenga heshima baina yenu na udugu uliokuwa bora. Utakaoepusha fitna na ugomvi baina ya ndugu na familia.

Na tambua ewe muislamu, uislamu haukuweka haya ila kwa maslahi. Kesi za shemeji zimezidi sana ndani ya jamii zetu. Tatizo sisi tuko mbali na maamrisho ya dini zetu na tumekumbatia mila za kikafiri. Nafsi ya mtu usiibebee dhamana.Kwani nafsi daima inaamrisha maovu. Allah (subhanahu wataala) anasema “Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu “ (Suratu Yuusuf : 53). Na huwezi kujua ni mbinu gani anazoweza kutumia sheytwan.

Ishi katika njia ya Allah ili upate furaha hapa duniani na kesho akhera.

No comments:

Post a Comment