Friday 24 October 2014

UKUMBUSHO KWA WENYE KUFANYA MIJADALA NDANI YA MITANDAO YA KIJAMII NA KUISHIA MATUSI AU KUZUA NDANI YA DINI

Makala Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wa ta‘ala) Muumba wa kila kilichomo katika ulimwengu huu. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Katika makala yangu ya leo nakusudia kupeleka nasaha zaidi kwangu binafsi pamoja na ndugu zangu wa kiislamu ambao hutumia mitandao ya kijamii kwa njia ya kujadiliana mambo mbali mbali ya kidini au ya kijamii.

Kumekuwa na maumivu makubwa ndani ya nafsi za waumini mbalimbali ambao huwa wanasoma maoni na mijadala ya dini ya waislamu ndani ya mitandao ya kijamii. Mijadala yenye hekima inafaa kwani inaleta funzo ndani ya jamii na kukosoana pale watu walipokosea. Ila mingi ya mijadala hiyo imekuwa haina heshima. Imekosa busara, na mwisho ni maneno machafu ambayo hata kuyaandika mfano wake siwezi. Leo nitajaribu kuyazungumza haya mambo kwa uchache ili tuweze kupeana tahadhari ili tusije kujuta siku ambayo mwanadamu hayatomfaa majuto yake. Miongoni mwa mambo yanayofanywa ni kama yafuatayo :

1-MATUSI YA NGUONI NA MANENO MACHAFU

Kwa hakika ukiwa unaangalia mijadala ndani ya facebook au whatsapp wengi wa watu huishia katika kutukanana na kutoleana maneno machafu. Ikiwa muislamu mwenzako hakubaliani na msimamo wako basi usimtukane wala usimwite majina mabaya au kumwambia maneno yasiyofaa. Tumia hekima katika kumfanya yule mtu aweze kukufahamu na aweze kukuelewa kile unachokikusudia. Lau angekuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam),masahaba zake na wema wengine waliopita kazi yao kutukanana tu katika kufikisha daawa kweli uislamu ungekuwa na hali gani?

Daawa yao na mijadala yao ilikuwa ni daawa iliyojengwa na misingi ya Allah (subhanahu wataala) iliyotajwa ndani ya Quraan “Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka”(16:125)

Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anaambiwa hata akijadiliana na wasiokuwa waislamu basi ajadiliane nao kwa namna iliyobora. Vipi baina ya muislamu kwa muislamu mwenzake? Vipi mazungumzo ya muislamu na muislamu mwenzake? Unadhani kuandika matusi na maneno yasiyofaa ndio utakuwa mtetezi wa uislamu? Hapana bali utakuwa ndio mpingaji wa aya za Quraan. Hebu tuangalie ndani ya Suratul Hujurati Allah ndani ya aya ya 11 Allah (subhanahu wataala) anasema “Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini.” Je haya yote waislamu tunayasahau?

Kumtukana muislamu mwenzako na asiyekuwa muislamu ni makosa ndani ya dini yetu. Tutumie lugha nzuri na laini baina yetu na baina ya wasiokuwa waislamu. Na yule ambae atakutukana basi wewe usirejeshe kwa tusi fahamu kuwa bado hajaijua haki siku akiiijua hatofanya hivyo.

Tuwe wapole na wenye kuheshimiana daima baina yetu.

2-KUZUSHWA KWA HADITHI ZA UONGO

Wakati watu wanapojadiliana wako watu huvuka mipaka na kuzusha yale yasiyokuwemo ndani ya dini. Wako wanaotunga hadithi na wako wengine wanaotoa fatwa kwa mambo wasiyokuwa na elimu nayo.

Ndugu zangu wa kiislamu tumuogopeni Allah (subhanahu wataala) tusitunge au tusiseme jambo ambalo halimo ndani ya Quraan wala sunna. Kama jambo hulijui ni bora kukaa kimya kuliko kuzua. Je unajua ni yapi yanayomsibu mwenye kuzua katika dini? Kutoka kwa Bibi Aisha(Radhiya Allahu anha) kuwa Mtume (Swalla Allahu alayhi wa aalihi wasallam) amesema : “Atakayezua akatia katika Dini yetu hii ambacho hakiko atarejeshewa mwenyewe.” (Al Bukhaariy na Muslim).

3-KUJITUKUZA KWA MTU KWA DHEHEBU LAKE AU ELIMU YAKE

Wako watu huwa wanajigamba na kujisifu kutokana na misimamo yake. Na huwa anaona ni rahisi sana kuwaambia waislamu wengine kuwa ni watu wa motoni na yeye na wenye kufuata madhehebu au misiamamo aliyokuwa nayo yeye ndio watu wa peponi na wako sahihi. Ni nani aliyekupa darja ya kuwaweka watu peponi na motoni? Ni nani aliyekwambia wengine uwadharau. Huo sio uislamu.

Tukhitalifiane lakini tusitoane kwenye uislamu wala tusiingizane motoni. Kwani hiyo ni kazi yake Allah (subhanahu wataala) peke yake. Bali sisi tukae kwa upendo nah uruma baina yetu. Allah (subhanahu wataala) anasema “Basi msijisifu usafi. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga na maovu.”(53:32).

Wako wengine wao hujiona ndio wenye elim una ndio wana haki ya kusema kila kit una wasemalo wao ndio sahihi ya wengine si sahihi. Huku ni kukosa kwa elim una adabu zake. Na inampasa muislamu ajiepushe na tabia hizo. Kwani kujionesha na kibri kuna makatazo makubwa ndani ya uislamu. Imepokelewa kutoka kwa Abdullah bin Masud (Radhi za Allah ziwe juu yake) kwamba Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema:"Hatoingia Peponi ambaye moyoni mwake mna chembe ya kiburi". Mtu mmoja akauliza: “Mtu hupenda nguo yake iwe nzuri na viatu vyake viwe vizuri (itakuwaje?)” Akasema: "Hakika Allaah ni Mzuri Anapenda Uzuri. Kiburi ni kukataa haki na kudharau watu)"Muslim

Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) :“Ninachokuogopeeni sana ni Shirki ndogo.)) Maswahaba wakauliza: "Ni nini hii Shirki ndogo, ewe Mtume wa Allah?" Mtume (Swalla Allahu alayhi waaalihi wasallam) akasema: Riya (kujionyesha).” [Imepokewa na Imaam Ahmad]

Nasaha zangu kwa waislamu tutumieni mitandao ya kijamii kwa uzuri. Daima tujue kuwa kila tunalolifanya linaandikwa na tutakuja kuyakuta katika kitabu chetu. Tuitumie mitandao hii kwa kujua kuwa Allah (subhanahu wataala) anatuona. Ikiwa binaadamu mwenzako unamuonea haya akuone ukiwa katika jambo ovu je huoni haya jicho la Allah likiwa linakuona unamuasi yeye na unafanya kinyume na alivyoamrisha?

Tutubieni kwa Allah (subhanahu wataala) toba ya kweli na tuache kabisa yale tuliyokuwa tunayafanya. Allah (subhanahu wataala) anasema “Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.”(50:19). Na anasema tena Allah (subhanahu wataala) “Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.”(36:65). Tukumbuke aya ya Allah (subhanahu wataala) isemayo ““Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.”(2:281).

2 comments: